MAMBO 15 NILIYOJIFUNZA MWEZI MEI

Habari mfuatiliaji wa blogu hii kila siku, kila siku huja na habari zake na zinaweza kuwa na athari chanya au hasi. Ni neema na jambo la shukrani kupata pumzi tena ya kuendelea kujifunza na kujiboresha kila siku ili muda unaopatikana utumike kukaribia ndoto zetu, malengo yetu na hata kazi zetu. Usiache kujifunza hata kama wakati mwingine siku imeanza ovyo au umepoteza hamasa ya kuendelea na kufanya lile ambalo umekua kufanya. Maisha ni kama darasa linalokupa somo kila siku, nikukaribishe rafiki, ndugu yangu na mfuatiliaji kujifunza mambo niliyojifunza mwezi Mei

  1. Mwanzo wa jambo huwa na hamasa kubwa sana kuliko muda unavyoenda zaidi, somo nililojifunza ni kutunza hamasa hii mpaka mwisho wa safari haijalishi njiani unakutana na kitu gani, itunze kama yai.
  2. Kila habari ivumayo sasa ni ya muda haitadumu kuendelea kuwepo, na hii inatia moyo kuwa ugumu au changamoto unayopitia ni ya muda ukiendelea kujituma na kutafutia majibu. Usipoteze sana muda litokealo hupita baada ya muda
  3. Usikae sana kufikiri kwa vitu ambavyo vipo juu ya uwezo wako, kukaa na kuvifikiri sana ni kujiumiza kihisia na kupoteza muda mwingi, kukaa na kutaka kurudisha jua kurudi nyuma ni kazi ambayo hutaiweza na kujisumbua sana. Huu ni mfano mdogo tu kuna mengi ambayo huna uwezo nayo yaache
  4. Kufeli sio mwisho wa kujaribu, bali ni kutafakari na kujitathimini wapi ulikosea na uanze kwa namna gani kuhakikisha awamu nyingine unafanya kwa uzuri
  5. Nyakati za mambo hayako sawa kwako usifikiri kuwa ndoto imeishia hapo, bado nafasi ipo kuendelea na safari ya kule unakotaka ufike, kupitia nyakati ngumu nako ni sehemu ya maisha usilaumu bali kubali na chukua hatua
  6. Wengi huacha kufanya walivyoanzisha sababu ya kutamani kupata mrejesho watu wanasemaje?, mtu huandika akitaka kuona mrejesho kaandikaje si kitu kibaya. Ila endelea kufanya sababu ni sahihi kufanya
  7. Ukijituma kwa kila kitu njia ya mafanikio huwa rahisi sana, endelea kujituma hata kama hali ya hewa ni mbaya
  8. Siku zinaenda sana hivyo jambo usemalo nitafanya kesho huenda muda ukapita na usiwe umefanya, jilazimishe kufanya leo leo maana muda una ukomo wake
  9. Kipindi cha ujana kina mambo mengi sana unapokosa msimamo thabiti mivumo yake ni rahisi sana kukupeperusha kama karatasi. Wekeza katika kujijua na pia katika imani ya kumwamini Mungu maana ni kipindi chenye hatari na heri pia
  10. Wengi ni wasemaji sana kuliko kuingia katika matendo, na hii kufanya miaka yote kubaki kama tulivyo pasipo kubadilika chochote.
  11. Majibu mengi yapo katika maarifa sahihi, siri ya mafanikio ipo katika maandishi. Ndo maana vitabu tukufu vina nguvu sana endapo yaloandikwa yakifuatwa maisha yetu yatakua ya ushindi kila siku.
  12. Ukiandika malengo yako katika maandishi karibu asilimia kubwa ukiweka nidhamu ya kuyasoma kila siku, kiwango cha kuyatimiza ni kikubwa sana kuliko yakibaki akilini, andika chini kama hatua ya mlango wa kutokea unachokifikiri.
  13. Maisha yana ukomo wake, na pengine huwa huja ghafla, hii itupe kujua muda tulionao sasa ni wa thamani zaidi kuliko huo tunaofikiri kesho. Maisha ni sasa na muda wa kutunza ni sasa.
  14. Usipochukua hatua na kutenda hakuna kitu kitabadilika, lawama hazisaidii kupunguza ugumu wa maisha au mambo. Ila kuchukua hatua ni msingi wa mabadiliko
  15. Kila kitu kipo kwa ajili yako na yangu kama utakubali kutoa gharama kukipataNikutakie tafakari nzuri ya haya mambo ambayo nimejifunza mwezi wa tano, nimekushirikisha ujifunze. Maana hakuna aliyefuzu kujifunza kila siku tunajifunza katika tusivyovijua na hata tunavyovijua. Nikutakie maandalizi mazuri juu ya mwezi unaokuja ikiwa tunaelekea nusu ya mwaka. Endelea kujituma na kujilazimisha katika malengo yako hata kama mambo ni magumu kwako, endelea kupambana

Na Raymond Nusura Mgeni (Malenga wa Ubena)

 

Leave a comment

Design a site like this with WordPress.com
Get started